Ni afunei kwa mayatima watatu wa Quincy Timberlake baada ya Wakenya wenye moyo safi kujitokeza kwa wingi na kuwachangishia Zaidi ya shilingi milioni moja.Hadithi ya mayatima hao iliibuka tena mwishoni mwa wiki jana ambapo wakili Wahome Thuku alipeleka mitandaoni na kusimulia hadithi yao na majanga ambayo yamekuwa yakiwakumba tangu baba yao kutoroka nchini miaka kadhaa iliyopita na kuwaacha mikononi mwa mama yao ambaye pia alisemekana kufariki mwaka jana.Kwa wale hawajui Timberlake, Mwaka wa 2009, jina la Quincy Timberlake liligonga vichwa vya habari kufuatia ufichuzi wa uhusiano wake na mwanahabari mlimbwende wa runinga Esther Arunga.
Timberlake ambaye alikuwa mwanaharakati wa kisiasa nchini alisemekana kuitelekeza familia yake na kuingia katika uhusiano wa mapenzi na Arunga na sakata lao lilipochipuka kipindi hicho, alilazimika kuficha uso wake mbali na nyumbani.Alisemekana kutorokea nchini Australia pamoja na Arunga huku akiiacha familia yake; mkewe Rose Mweni na wanao watatu Trivor, Quicy na Cassidy.Inaripotiwa kwamba tangu kipindi hicho alipotorokea Australia, Timberlake hakuwahi kurudi nchini kuifuatilia familia yake, na aliwaacha katika umaskini mkubwa,Mweni akilazimika kujukumika kama baba na mama ili kukimu mahitaji ya wanao watatu.
Kulingana na ripoti iliyochapishwa na Thuku, mtoto mkubwa, Trevor alilazimika kuvaa viatu vilivyoachwa na mama yake baada ya kifo chake mwaka jana na kulazimika kuwatafutia wadogo zake riski ya kila siku.Wadogo zake wawili wamekuwa wakihangaika hapa na pale shuleni kutokana na gharama kubwa ya maisha na elimu kwa wakati huo huku wakiishi katika nyumba moja chakavu jijini Nairobi waliyokabidhiwa na mhisani mwema baada ya kufukuzwa kutoka nyumba ya kupanga walikoachwa na mama yao kutokana na kurundika kwa kodi ya kila mwezi.
Kufuatia hadithi hii ya kuhuzunisha, Wahome Thuku aliwaomba watu wenye moyo wa kusaidia kujitokeza ili kuwasaidia vijana hao watatu ambao wanasema hawakuwahi kusikia tena kutoka kwa baba yao tangu alipotoka nchini Ghafla, na hata hawana uhakika kama habari za msiba wa mama yao zilimfikia kule aliko.Kuelekea Wikendi, Wakenya wengi walioguswa na simulizi hiyo ya uhalisia walijitokeza kwa wingi na kutoa michango yao na kufikia Jana, Thuku kwa furaha akifunga michango hiyo alisema kwamba wanamitandao walichangisha Zaidi ya shilingi milioni moja kwa ajili ya kuwasaidia vijana hao