Home NEWS Haifai Kuweka Shule Za Chekechea Pamoja Na Zile Za Msingi

Haifai Kuweka Shule Za Chekechea Pamoja Na Zile Za Msingi

0

  

Kamati iliyoteuliwa na Rais William Ruto kuchunguza na kutoa mapendekezo yake kwa serikali hatimaye ilikamilisha kazi yake na kumkabidhi rais mapendekezo hayo juma lililopita.Mapendekezo hayo yalikuwa mazuri na kusifiwa kwa kazi njema waliyofanya.Hata hivyo, miongoni mwa mapendekezo hayo ilikuwepo moja ambalo lilisema kuwa shule za chekechea zijumlishwe pamoja na zile za msingi chini ya usimamizi mmoja wa mwalimu mkuu mmoja.

Kwa mtazamo tu, mwalimu mkuu wa shule ya msingi husimamia madarasa manane. Ikiwa pendekezo la kamati hii litatiliwa maanani, ina maana kuwa mwalimu mkuu wa shule ya msingi atakuwa akisimamia madarasa kumi au kumi na moja katika baadhi ya sehemu; kutoka darasa la vikembe hadi la tisa.Ni wazi kuwa huu ni mzigo mkubwa na mzito kwa mwalimu mkuu na unaweza kuvuruga utendakazi kwa kiasi kikubwa. Baadhi ya shule za msingi zina wanafunzi zaidi ya elfu moja.Kuongezewa tena darasa la tisa, chekechea na vikembe kwa walio mjini ni jambo la kusumbua akili.

Tayari walimu wakuu wengi wa shule za msingi wanashindwa na kuzitawala ipasavyo kwa sasa, sembuse wakiongezewa madarasa?Isitoshe, katiba ya sasa inaweka madarasa ya chekechea chini ya uangalizi wa kaunti.Ingawaje kumekuwa na tatizo la usawazishaji wa mishahara ya walimu wa chekechea katika kaunti mbalimbali, pendekezo hili likichukuliwa litahitaji kuwepo kwa urekebishaji wa katiba.Huenda hili likazua mvutano kati ya serikali kuu na serikali za kaunti.Jambo jingine muhimu linalofaa kuangaziwa kwa kina ni changamoto za kuwachanganya watoto hawa wa chekechea na wale wakubwa.Kuna matumizi yao ya vyoo, chakula na hata michezo. Haya yote yanafaa kuangaliwa kwa karibu sana. na mwalimu asiye na majukumu mengine makubwa ili aweze kufanikisha malengo ya elimu ya watoto hawa.

Ikiwa utaratibu huu wa kuweka shule za chekechea pamoja na zile za msingi, basi itabidi walimu wakuu wapewe manaibu wawili au zaidi ili mmoja ateuliwe na kupewa jukumu la kusimamia shule za chekechea.Hii ni kwa sababu watoto hawa wadogo wanahitaji uangalifu wa karibu sana kwa kuwa bado hawajakomaa na kupata viungo thabiti vya kuwawezesha kuingiliana na wale wakubwa.Kwa kuwa hawa ni mapendekezo ya kamati tu, pana haja ya baadhi ya mapendekezo hayo yapigwe darubini kabla ya kutekelezwa wala wasitekelezwe tu pasi kuchujwa ili kutoa yale yanayoweza kuleta utata au changamoto zaidi katika utekelezaji wake.Wanatakiwa Kila la heri kwa rais na mawaziri wake wakijadili mapendekezo haya.

Previous articleMayatima waliotorokwa na baba baada ya kifo cha mama wachangiwa zaidi ya 1m mtandaoni
Next articleKibera Girls Na Soccer Assassins Vitani Kutafuta Mshindi Wa Divisheni Ya Kwanza